Mhe. Hemed ataka mrundikano kesi udhalilishaji umalizwe

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka watendaji wa serikali kuwajibika ipasavyo ili kumaliza mrundikano wa kesi za udhalilishaji nchini.

Mhe. Hemed alitoa agizo hilo katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa Serikali wanaoshughulikia masuala ya udhalilishaji huko ofisini kwake Vuga Jijini, Zanzibar.

Alisema taasisi zinazosimamia kesi za aina hiyo, zina watendaji wenye ujuzi na uzoefu ambapo uwajibikaji wao utasaidia kutokomeza janga la udhalilishaji nchini.

Aidha Mhe. Hemed alieleza jamii ya Wazanzibari inaimani na Serikali yao endapo kesi hizo zitafikia mwisho, pia zitasaidia Zanzibar kuwa Salama na yenye maendeleo.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed alisema ucheleweshwaji wa kesi hizo, unakosesha uvumilivu kwa wananchi kwa kuwakosesha imani za kwa Serikali yao hali aliyoieleza haifurahishwi kwenye awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa Serikali haifurahishwi kuona watuhumiwa wa kesi za udhalilishaji wanarundikana wengine kurejeshwa rumande bila kesi zao kumalizwa, na nyengine zikiwa za muda muda mrefu ambazo ni kinyume na haki za kibinadamu.

 “Nina uhakika kuna kesi zaidi ya miaka mitano hazijesha, kama zipo jamii inavunjika moyo hili linachangia jamii kutotoa ushahidi baadhi yao wakiamini hakuna kinachofanyika, tuache tabia hiyo” Alionya Mhe. Hemed.

Aidha, Mhe. Hemed aliendelea kuwasihi watendaji hao kutotumia kesi hizo kwa kumuonea mtu au kumpendelea yoyote bali watende haki kwa kusimamia viapo walivyoapa kumsaidia Rais wa Zanzibar katika kufanikisha majukumu yao ya kila siku.

“Wahusika wakiona mtu anaonewa tusimamie apate haki yake, tusimuonee mtu wala kumpendelea na isiwe kesi hizi ni sehemu ya kujipatia fedha” alitahadharisha.

Sambamba na hayo, Mhe. Hemed, aliwataka watendaji hao kuwa wawazi kwa kueleza changamoto zinazowakabili akitolea mfano uhaba wa rasilimali watu na vitendea kazi, magari ya kuwapeleka mahabusu na changamoto nyengine ili Serikali itatue changamoto hizo kwa wakati.

Kwa upande wake Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Awadh Juma Haji aliahidi kuwa Jeshi la Polisi litaendelea na kuwasaka wahusika wa vitendo vya udhalilishaji pamoja na mashahidi ambao wanakataa kufika mahakamani kutoa ushahidi kwa makusudi au kwa muhali.

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi halifurahishwi na  tabia ya baadhi ya waathirika wa kesi za udhalilishaji kujaribu kuweka mazingira kwa kumsaidia mlalamikiwa na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha ili kumaliza janga hilo nchini.

Nae Naibu Mrajis wa Mahkama kuu Zanzibar, Salum Hassan Bakari alieleza kuwa Mahkama imeweka mikakati madhubuti ya kuungana na Rais Dkt. Mwinyi kuhakikisha wimbi la udhalilishaji nchini linamalizika.

Akitolea mfano kesi zinazosikilizwa kwa wakati pamoja, nakupitiwa majalada ili kuona kesi zilizochukua muda mrefu, zinamalizwa kwa wakati.

Aidha, Naibu Mrajis alieleza Mahkama imeshatatua changamoto ya malipo kwa mashahidi hasa wataalamu ili watoe ushirikiano wa kutosha katika kuendesha kesi za udhalilishaji.

Kikao kazi hilichowakutanisha wadau kutoa Jeshi la Polisi, Mahkama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Wizara ya jamii, wazee, jinsia na watoto na Wizara ya Afya kilifanyika ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Vuga mjini Unguja.

@@@@@@@@@@

Ander Herera wa Manchester United apata ubalozi wa utalii, Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amekutana na kufanya mazungumzo na kiungo wa Timu ya PSG ya Ufaransa ambae aliwahi kuwa Mchezaji wa Timu ya Manchester United, Ander Herera katika Ofisi zake zilizopo Baraza la Wawakiishi, Chukwani Zanzibar.

Katika hafla hiyo Mhe. Hemed alimpongeza mchezaji huyo kwa kuja kutalii Zanzibar na kumtaka kuitangaza Zanzibar kiutalii.

Aidha, Mhe Hemed alimkabidhi Cheti cha Ubalozi wa Utalii mchazaji huyo, kwa niaba ya Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, alizungumza na watendaji wa Serikali wanaoshughulikia masuala ya udhalilishaji huko ofisini kwake Vuga Jijini, Zanzibar. (Picha na OMPR).

Leave a Reply

Your email address will not be published.