Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ameitaka jamii ya Zanzibar kuweka nguvu ya pamoja kwenye suala la malezi 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ameitaka jamii ya Zanzibar kuweka nguvu ya pamoja kwenye suala la malezi yanayoendana na mila na silka za kizanzibari ili kukuza taifa lenye tija na maarifa kwaajili ya maaendeleo ya baadae.

Alhajj Hemed aliyasema hayo huko Masjid Rahman Tomondo Wilaya ya Magharibi “B” Unguja wakati akijumuika pamoja na waumini wa kiislamu kwenye ibada ya sala ya Ijumaa.

Alisema jamii ya Zanzibar inasifika kwa ustaarabu na maadili mema ya asili ya watu wake yanayotokana na hulka na tamaduni tokea enzi za asili zao za ukarimu na kuheshimiana.

Alhajj Hemed alieleza mpromoko wa maadili kwa vijana unachangia kupata taifa lililokosa maarifa na nguvu kazi ya taifa.

Alisema vitendo viovu kwenye jamii vinahitaji nguvu ya pamoja ili kuvitokomeza na kutoa fursa kwa Serikali kutekeleza wajibu wake wa kuwatumika wananchi wake.

“Hatuwezi kuwa na taifa bora kama hatuna vijana imara wenye maadili mema na tunapaswa kusimama imara Wazanzibari hili sio la serikali pekee, niwaombe tusaidiane” aliasa Alhajj Hemed.

Sambamba na hayo, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kuiombea Nchi kuepukana na majanga na maradhi mbali mbali ambayo yanachangia kuzorotesha shughuli za maendeleo nchini.

Akilizungumzia suala la mafuta, Alhajj Hemed alieleza kuwa Serikali imepunguza gharama za bei ya mafuta ili kuwapa unafuu wananchi wake katika kupata huduma hiyo na kupunguza ukali wa maisha.

Kwa upande wake, Ustadh Muhamed Salum katika Khutba yake amewataka waumini wa dini ya kiislam nchini, kuzingatia historia za Mitume akitolea mfano Sira ya Nabii Ibrahim (A.S) kuhama mji kwa ya ajili Allah (S.W) pamoja na uaminifu katika masuala mbali mbali ya jamii.

Aidha, Ustadh Muhamed aliwataka wazazi na walezi kuandaa mazingira mazuri ya kupata familia bora kwa kuowa wake wema kama dini ilivyoeleza wa ustawi wa jamii zilizobora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *