Uchumi wa bluu kuengeza kipato zaidi ya 60% – Mhe. Hemed

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali kupitia Sekta ya Uchumi wa Buluu itasaidia kukuza kipato cha nchi kwa zaidi ya Asilimia 60 hatua aliyoieleza kuwa itasaidia Zanzibar kufikia malengo yake ya maendeleo iliyojiwekea.

Mhe. Hemed alisema serikali imeelekeza nguvu zake katika sekta hiyo ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla aliyasema hayo wakati alipokutana na timu ya Umoja wa Ulaya (EU) iliyofika Ofisini kwake Vuga, mjini Unguja kwa lengo la kujua hali ya Uchumi wa Zanzibar na maendeleo yake, chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

 Alieleza Sekta ya Uchumi wa Buluu imejumuisha fursa nyingi zikiwemo Utalii, Uchimbaji wa Mafuta na Gesi pamoja na uvuvi.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed alieleza wananchi wa Zanzibar wananufaika kwa fursa nyingi za ajira zinazosaidia kukuza vipato vyao, viwanda pamoja kukuza biashara za ndani na nje ya nchi.

Kuhusu hali ya siasa za Zanzibar, Mhe. Hemed alisema Zanzibar ipo kwenye hali nzuri ya amani na utulivu, chini ya miongozo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi nakuongeza kuwa, ushirikishwaji wa vyama vinavyounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini ni wa kuridhisha akitolea mfano uwakilishi kwenye wajumbe wa Baraza la Mapinduzi.

Aidha, alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kupokea maoni kutoka kwa wadau mbali mbali wa vyama vya siasa yenye maslahi na Wazanzibari kwa kuzingatia Sheria na kanuni zilizopo.

Pamoja na mambo mengine, Mhe. Hemed alieleza kuwa Serikali imezingatia usawa wa kijinsia katika nafasi mbali mbali za uongozi ili kuendana na kasi ya dunia ilivyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri kwa Afrika kwenye nchi zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) Bi. Yamina Guerfi alieleza ujio waom kwa Zanzibar ni kujua maendeleo na mikakati iliyopo kwa maslahi ya Wazanzibari.

Hata hivyo, alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Umoja wa Ulaya (EU) utaendeleza ushirikiano uliopo baina yao na Tanzania na kueleza kufurahishwa kwao na mwendelezo uliopo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoundwa kwa mfumo wa Umoja wa Kitaifa akitolea mfano Amani na ulituvu uliopo.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akizungumza na timu ya Umoja wa Ulaya (EU) iliyofika Ofisini kwake Vuga, mjini Unguja kwa lengo la kujua hali ya Uchumi wa Zanzibar na maendeleo yake, chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *