Dkt. Mwinyi aipongeza NMB kuwainua wananchi kiuchumi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza benki ya NMB kwa kuanzisha Programu mbali mbali walizozilenga kuwanufaisha Wananchi.

Dkt. Mwinyi ameeleza hayo kupitia Hotuba iliyosomwa kwaniaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika uzinduzi wa Jukwaa la “Go na NMB” uliofanyika huko Viwanja vya Bustani ya Forodhani, Jijini Zanzibar.

Ameeleza hatua iliyochukuliwa na benki ya NMB kuanzisha Jukwaa hilo inalenga kutoa mikopo na vitendea kazi kwa vijana ambao wataweza kujiajiri kupitia  fani mbalimbali zikiwemo uvuvi, boda boda na mama lishe.

Alisema hatua hiyo itasaidia  kutatua changamoto za kupata mitaji nakuongeza kuwa ukosefu wa mitaji unakwamisha malengo ya wananchi kujiajiri.

Sambamba na hayo Rais Dkt. Mwinyi alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kwa dhati kuboresha na kuendeleza elimu ya fedha katika ngazi zote ili kuwajengea wananchi uwelewa wa masuala ya kibenki.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alieleza fursa zilizopo katika Jukwaa hilo zitasaidia kuondosha tabia za baadhi ya Kampuni zenye kujipatia kipato kupitia nguvu za Wananchi kwa kutumia mwanya wa kukopesha na hatimae   kuwatapeli Wananchi.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alieleza lengo la kuanzishwa Programu hiyo ya Go na NMB ni kuwaweka karibu vijana katika Jukwaa moja kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane katika kukuza Uchumi wa Nchi.

Alisema zaidi ya Asilimia Sitini ya Watanzania ni Vijana jambo ambalo limepelekea NMB kuelekeza nguvu hizo kwao kwa kuzalisha ajira na kusaidia kujikwamua kiuchumi.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Rashid Simai Msaraka alieleza NMB imeonesha kuunga Mkono Azma ya Serikali kukaribisha Taasisi binafsi kuungana na Serikali katika kuwaletea maendeleo Wananchi wake.

Aidha, Mhe. Msaraka ameeleza, Jukwaa hilo litawasaidia Kina Mama na Vijana kujipatia mikopo nafuu itakayowasaidia kujipatia kipato na kujikwamua kimaisha na kuisaidia Serikali katika kuwawezesha wananchi wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *