SMZ yathamini michango mashirika ya umma na binafsi: Mhe Hemed
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameeleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini Mchango wa Mashirika ya Serikali na taasisi binafsi kwenye Maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi katika kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa maendeleo ya Zanzibar.
Mhe. Hemed ameeleza hayo kwenye hafla ya uchangiaji wa rasilimali za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 iliyofanyika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua umuhimu wa Mashirika hayo kwa kuwashirikisha moja kwa moja katika Suala la uchangiaji wa Rasilimali za kufanikisha zoezi hilo.
Mhe. Hemed ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi alisema uhitaji wa vifaa na rasilimali Fedha, Jumuiya ya Wafanyabiashara, asasi za kiraia na wadau wengine wamekuwa mstari wa mbele kwa kuiunga mkono Serikali kwa kuleta michango mizuri katika utekelezaji wake.
Aidha, altumia fursa hiyo kuwapongeza Jumuiya ya Wafanyabiashara na Mashirika ya Serikali na Binafsi kwa kuchangia Rasilimali mbali mbali kwa lengo la kufanikisha Utekelezaji wa Zoezi hilo.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed alieleza Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi lina umuhimu Mkubwa kwa kuiwezesha Serikali na wadau mbali mbali kupata Hisabu halisi ya Idadi ya Watu Nchini pamoja na taarifa zao za kijamii, kiuchumi na makazi yao.
Alieleza matokeo yatakayopatikana kwenye Sensa yatasaidia kupata takwimu sahihi katika kufanya maamuzi ya kuleta maendeleo ya taifa.
“Takwimu hizi zitasaidia katika kutathmini utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo wa Muda wa kati wa Zanzibar wa Mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 , ikiwa ni Utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050 ambao unalenga katika Uchumi wa Buluu kwa ukuaji Jumuishi na Maendeleo endelevu na Mipango mengine ya Kimataifa “
Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed aliwahakikishia Wadau hao kwamba rasilimali zitakazokusanywa zitatumika kama ilivyokusudiwa ili kufanikisha zoezi hilo kwa ufanisi wa hali ya juu.
Nae Waziri wa Nchi Afisi Ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma alieleza uelewa wa Wananchi kuhusu Sensa ni mkubwa kutokana na uhamasishaji uliofanywa tokea mwanzo wa mwaka huu hatua ambayo inaashiria kukamilika vyema zoezi hilo.
Mhe. Hamza alieleza zoezi la mwaka huu linafanyika kidigitali kwa kuwawepesishia wakaazi na watendaji wa Sensa kukamilisha zoezi hilo kwa wakati.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar, Hamad Hamad alieleza ushirikiano wanaopewa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikishwa katika hatua zote za maandalizi ya Sensa mwaka ya huu na kueleza kufurahishwa kwao kuona zoezi hilo litawarahisishia wananchi kupata biashara kirahisi kwa kutumia mfumo wa Anwani za Makazi.

ReplyForward |