SMZ, SMT kushirikiana kiutendaji

SERIKALI za SMZ na SMT zimesema zimekusudia kuimarisha na kuendeleza mazuri yote yanayotekelezwa na viongozi wa serikali hizo kuwafikia wananchi wa pande mbili za Muungano wa Tanzania.

Akizungumza kwenye kikao cha pamoja cha ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma alisema, kufanyika kwa vikao kama hivyo kati ya pande mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kutaendeleza kuimarisha umoja na Muungano uliopo baiana yao katika kuwafikishia wananchi maendeleo ya taifa lao.

Aidha, alisema vikao hivyo pia vitasaidia kuondosha kero za wananchi zinazolalamikiwa kila siku kufuatia changamoto zinazowakabili wananchi wa pande mbili hizo za Muungano kwa kuendelea kuzitafutia ufumbuzi wa kuzitatua.

Alisema vikao kama hivyo huleta tija kwenye upangaji wa mikakati na mipango ya maendeleo ya kazi kupitia viongozi wa pande hizo sambamba na kubadilishana uzoefu wa kazi wanazozifanya kila siku.

Aidha, Mhe. Hamza aliongeza vikao hivyo, vinasaidia kujenga uzoefu na kusaidia kuimarisha Muungano, pamoja na kuenzi mawazo ya waasisi wa taifa la hayati Julias Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani karume pamoja na kuboresha maendeleo ya wananchi.

Sambamba na hayo, alieleza watapitisha rasimu ya ratiba ya vikao vyao baina ya ofisi mbili hizo kwa mwaka 2022/2023.

Pamoja na hayo, alisema watapokea taarifa fupi ya maandalizi ya taarifa ya serikali ya SMT na SMZ kuhusu utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa kipindi cha miaka miwili 2020-2022.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Boniface Simbachawene, alisema kupitia kikao hicho walijadili masuala mbalimbali yanayohusu Muungano na maendeleo ya nchi.

Alisema kikao pia kilijadili masuala yasiyohusu Muungano ambayo yaliorodheshwa kwenye kikao hicho nakujadiliwa na kueleza kwamba yatafanyiwa kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano wa hali ya juu.

Alisema kukutanika kwao ni maagizo ya viongozi wakuu, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambao walitaka ushirikiano uwepo kati ya viongozi wa ofisi mbili hizo, lengo la kubadilishana uzoefu wa kazi na kuimarisha umoja uliokuwepo.

“Viongozi wetu wamesisitiza tuwe tunafanya kazi kwa ushirikiano wa hali ya juu. Kazi zetu, hatuwezi kuziepuka kwani ni chama kimoja ambapo tumekuwa tunatekeleza ilani ya CCM kwa pamoja, baadae lazima tukatoe taarifa katika chama chetu katika kutekeleza ilani hii” alisema.

Hivyo, aliwataka watanzania kuendelea kuishi kwa upendo na kutobaguana kwani umoja ndio unaoleta maendeleo katika taifa sambamba na kuimarisha muungano uliokuwepo kwani ndio tunu ya Taifa.

Katika kikao hicho, Viongozi hao, waliokuwepo chini ya Mawaziri wawili wa SMT na SMZ, wamepokea taarifa ya utekelezaji wa masuala yaliyojadiliwa katika kikao cha masharikiano baina ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, ngazi ya makatibu wakuu cha Julai 1 mwaka 2022 kilichofanyika jijini Dodoma.

Kikao hicho kwa upande wa ofisi Makamo wa Pili wa Rais ni cha kwanza kwa upande wa mawaziri ambapo ni fursa pekee ya kuona masuala ya muungano ya kiutendaji yanaendelea kuimarika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *