WAZIRI JENISTA ATEMBELEA  MRADI WA MAMA NA MTOTO DONGE PWANI

SERIKALI ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itaendelea kushirikiana na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha wanawasaidia wananchi wasiojiweza kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini (TASAF), ili kuona hali zao zinaimarika kama zilivyokuwa za wengine.

Akizungumza na walengwa wa shehia ya Kianga katika ziara yake ya kukagua miradi ya TASAF, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utwala Bora, Jenista Mhagama,alisema Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wamekuwa wakifanya kazi kwa njia mbalimbali ili kuona taifa la Tanzania linaendelea kuwa bora na maendeleo yanawafikia wannachi wote.

Alisema, viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi kubwa kupitia miradi mbalimbali ikiwemo Tasaf kwa kuwanufaisha wananchi moja kwa moja ikiwemo kuwawezesha kiuchumi sambamba na masuala ya afya hasa kwa Mama na watoto.

“Miradi mbalimbali imekuwa ikiletwa ili hali za wananchi wanaoishi katika kaya masikini waweze kupata maendeleo kupitia miradi yao wanayoianzisha” alisema.

Aidha alisema, kupitia viongozi hao, Taifa linaendelea kusonga mbele kwani mabadiliko makubwa yanaonekana katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, kupitia Royal Tour ambapo viongozi hao walijitoa wenyewe kufungua utalii na matokeo yake ni yanaonekana.

Hata hivyo, aliwataka wanakaya kuendelea kuwahamasisha watoto wanaotokana na kaya zao kuhudhuria vizuri kwenye masomo yao kwa ngazi zote kuanzia maandalizi na msingi kwa kuhakikisha wanakwenda skuli na vyuo kwa ujumla.

“Tuhakikishe watoto wetu wasome katika ngazi mbalimbali na waliofika kwenye vyuo vikuu waweze kupatiwa mikopo kupitia serikali yetu” alisema.

Hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kuwaunga mkono viongozi hao kwani wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii ili kuona wanawapelekea maendeleo wananchi wao.

“Wanufaika wa TASAF tutokeni mbele kutoa shukrani zetu za dhati kwa viongozi wetu kwani wamekuwa wakifanya kazi kwa wananchi wote bila ya ubaguzi” alisema.

Alisema makusudio ya serikali zote mbili ni kuona wananchi hasa walengwa wa TASAF wanaendelea kufaidika kupitia mradi huo.

Hata hivyo, aliwaagiza watendaji wa TASAF kwenda kufanya uhakiki kwa wanakaya wanaofaidika na mfuko huo ili kuepusha changamoto zilizokuwepo kwa wanufaika wao.

“wakati Mwengine tunaweza kuingiza watu waliokuwa vigezo vyao havijatimia na kuwaacha watu waliokuwa na hali duni ambapo walistahiki kuingia kwenye mradi huu hivyo tusipuuze tuende tukawahakiki tena” alisema.

Sambamba na hayo, aliwapongeza viongozi wa jimbo la Mwera kwa kushirikiana na serikali zao pamoja na viongozi wa Tasaf kwani wamekuwa wakitekeleza kwa vitendo miradi inayopelekwa kupitia tasaf.

Nae, Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Salinina, alisema, serikali zote mbili zinafanya kazi kutokana na muungano uliokuwepo ambapo miradi mbalimbali yamekuwa wakifanywa kwa pamoja ikiwemo mradi wa TASAF.

Nae, Mwakilishi wa Jimbo la Mwera, Mihayo Juma N’hunga, alisema ataendelea kushirikiana na serikali katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na kusimamia miradi inayoanzishwa katika jimbo lake.

“Hatuna budi kuungana na serikali yetu inayoongozwa na chama cha mapinduzi, kwani wananchi wa jimbo lake wamekuwa wakifaidika na jitihada hizo ambapo wamekuwa na miradi mbalimbali” alisema.

Hata hivyo, alimuomba Waziri huyo, kuwajengea hospitali kwa ajili ya mama na mtoto ili kuona wamama wa kianga wanajifungua katika kituo cha afya kilichopo katika shehia iliyopo katika jimbo hilo.

Akisoma risala kwa wanakaya wa shehia ya Kianga, Nuru Abubakari Mohammed, alisema, katika mpango huo, wameweza kuanzisha vikundi mbalimbali vya wajasiriamali, ambapo vinaendelea kuwasaidia katika kujikimu kimaisha.

Aidha alisema, katika utekelezaji wa mpango huo, shehia hiyo imepata mafanikio ambapo walengwa wamekuwa na matumaini makubwa ya kukuza uchumi wa

kaya zao na taifa kwa ujumla

.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hamza Hassan Juma akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejiment  ya Utumishi wa Umma na Utawala bora wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania Mhe Jenista J. Mhagama  wakati alipofika Kujitambulisha Ofisini kwake Vuga Kwa Ziara Maalum ya Kutembelea vituo vya Utekelezaji wa Mradi wa TASAF

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *