MHE. HEMED ASISITIZA KUTHAMIWA KWA KAZI ZA WASANII KUTOKANA NA MCHANGO WAO KWA TAIFA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amezitaka taasisi mbali mbali na jamii kwa ujumla kuthamini kazi nzuri inayoendelea kufanywa na wasanii Nchini kutokana na mchango wao katika kufanikisha maendeleo ya taifa.Mhe. Hemed ameleza hayo wakati akizindua rasmi tamasha la kwanza la washairi Tanzania lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar. Amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa washairi nchini kutokana na kazi yao nzuri ya kufikisha ujumbe jamii ikiwemo kupinga vitendo vya udhalilishaji kupiga vita madawa ya kulevya pamoja na kutoa elimu kuhusiana na masuala ya Afya.Ameleza kuwa mchango huo unaotolewa na wasanii ikijumuisha wasanii wa utanzu wa mashairi imepelekea Serikali zote mbili kuunda Wizara maalum zinazohusiana na Utamadun, sanaa na Michezo katika kuhakikisha kuwa tasnia hiyo zinapiga hatua.Akizungumzia suala la kuhifadhi kazi za wasanii Makamu wa Pili wa Rais amezitaka Jumuiya za Hakimiliki COSOTA na COSOZA kusimamia vyema kanuni ziliopo za ukusanyaji wa mirabaha kutoka kwa watumiaji wa kazi za sanaa ili wasanii wanufaike na matunda ya kazi zao. Kuhusiana na changamoto zinazowakabili washairi hao Mhe. Hemed ameutaka uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha kuwa wanakaa pamoja na washairi hao ili kuzimaliza changamoto zote hasa ile ya kukosa ofisi za kudumu huku akisisitiza serikali ya awamu ya nane itaendelea kuikuza sanaa ya ushairi.Nae Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Mhe. Tabia Mauid Mwita amewapongeza washairi kwa kuandaa tamasha hilo hali iyo iliopelekea kurudisha hadhi ya mashairi nchini na kuwataka washairi hao kuiga na kusoma kupitia washairi waliotangulia.Kwa upande wake mwenyekiti wa umoja wa washairi Tanzania (UWASHATA) Bwana Hassan Ligile amesema tamasha hili litakuwa endelevu ambapo kila mwaka hali itakayosaidia kurudisha hadhi ya mashairi nchini.Akisoma risala ya washairi Ndugu Said Suleiman Ali ameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuziomba taasisi husika za kumbukumbu na historia kuzitambua kazi za washairi na kuzitunza ili kukuza Idara ya Nyaraka kwa lengo la kuacha athari kwa kizazi cha sasa na baadae.Kupitia tamasha hilo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amezindua kazi mbali mbali za watunzi wa mashairi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara ambazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa Jamii.Kauli mbiu ya Tamasha hilo inasema Ushairi wa Kiswahili ni rasilimali yetu tuutunze.

Leave a Reply

Your email address will not be published.