Historia

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais imeanzishwa kwa lengo la kuratibu majukumu ya Makamu wa Pili wa Rais kwa mujibu wa Katika ya Zanzibar ya Mwaka 1984. Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar (OMPR) imeanzishwa mwaka 2010 kufuatia marekebisho ya kumi na moja (11) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 toleo la 2010, kifungu Namba 39 (1) ambacho kinaeleza kuwepo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae atakuwa ni Msaidizi na Mshauri Mkuu wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kutekeleza kazi zake za kila siku.  Aidha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ndie Mratibu na Kiongozi Mkuu wa Shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi.

Kabla ya marekebisho hayo kazi na majukumu ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar yalikuwa yakifanywa na Waziri Kiongozi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1979 Toleo la 1984 ambapo nafasi hiyo ilikuwepo hadi kufikia mwaka 2010.  Zanzibar imekuwa na Mawaziri Kiongozi watano (5) katika awamu nne (4) kama ifuatavyo; Waziri Kiongozi wa mwanzo wa Zanzibar ni Mheshimiwa Ramadhan Haji Faki aliekuwa Waziri Kiongozi kwa kipindi cha miezi….. chini ya Rais wa Awamu ya Pili (2) wa Zanzibar Mheshimiwa Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi hadi hapo walipojiuzulu kwa pamoja nyadhifa zao mwezi … mwaka 1984 kufuatiliwa kuchafuka kwa hali ya kisiasa nchini. Maalim Seif Sharif Hamadi alikuwa Waziri Kiongozi wa Pili wa Zanzibar kuanzia mwaka 1984 hadi 1985 chini ya Rais wa awamu ya Tatu (3) ya Zanzibar kwa wakati huo Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi na baadae mwaka 1985 chini ya Rais wa Awamu ya Nne (4) ya Zanzibar Mheshimiwa Marehemu Mzee Idrissa Abdul-Wakil Nombe hadi mwaka 1987 alipovuliwa nyadhifa zote alizonazo za Chama na Serikali kufuatia uasi wa vuguvugu la kisiasa. 

Waziri Kiongozi watatu (3) wa Zanzibar ni Mheshimiwa Marehemu Dkt. Omar Ali Juma ambae aliteuliwa kushika wadhifa wa Waziri Kiongozi kuanzia mwaka 1987 katika Serikali ya Awamu ya Nne(4)  na kuteuliwa tena katika Serikali ya Awamu ya Tano (5) chini ya Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Salmin Amour Juma kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka 1995 alipoteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2000 nafasi ya Waziri Kiongozi ilishikiliwa na Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal. Katika Kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita (6) iliyoanza mwaka 2000 hadi 2010 nafasi ya Waziri Kiongozi wa Zanzibar ilishikiliwa na Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha ambaye ndie Waziri Kiongozi wa mwisho kabla ya kufanyika marekebisho ya 11 ya Katiba ya Zanzibar hapo mwaka 2010 na kuwepo Serikali ya Umoja wa Kitaifa na  kuanzishwa kwa nafasi za Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye ni Kiongozi kutoka Chama cha Upinzani kilichopata kura nyingi na Makamu wa Pili wa Rais ambae atatoka katika chama kilichoshinda uchaguzi.

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni miongoni mwa taasisi muhimu sana kwa Serikali kwani ndio iliyopewa jukumu Kikatiba la kuratibu na kuwaunganisha moja kwa moja wananchi na Serikali yao. Katika utekelezaji wa majukumu yake Ofisi hushirikiana na sekta nyengine katika kutoa huduma bora kwa wananchi ili kupunguza umasikini, kuwaletea maendeleo na kukuza uchumi wa nchi kwa ajili ya kutekeleza dhamira na malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Ofisi hii pia ni kiungo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.