MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR MHE. HEMED SULEIMAN ABDULLA AKIFUNGUA KONGAMANO LA MAADHIMISHO YA MIAKA 40 YA JUMUIYA YA MAENDELEO KUSINI MWA AFRIKA (SADC)

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeipa kipau mbele sekta ya uchumi wa buluu unaoelekeza matumizi mazuri na endelevu ya rasilimali ya bahari ili wananchi wake waondokane na umaskini.

Mheshimiwa Hemed, alieleza hayo wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya miaka 40 ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Kampasi ya Utalii Maruhubi.

Alisema kupitia kongamano hilo kuna haja kwa washiriki kujadili kwa kina namna bora ambayo Zanzibar itaweza kutekeleza kipau mbele hicho kwa kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu kupitia jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika (SADC)

Makamu wa pili wa Rais alileza kuwa ni jambo la kujivunia hivi sasa kuona kuwa zipo baadhi ya nchi zimeanza kufanya biashara na Zanzibar kupitia sekta hiyo akitaja nchi ya Congo kupitia wafanyabiashara wake wanaofika Zanzibar kujinunua bidhaa, hivyo ametoa wito kwa nchi nyengine zilizomo katika jumuiya ya SADC kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

“Uzoefu unaonesha kuwa wafanyabiashara wetu wengi wanaelekeza macho yao Dubai, India na China tu, inawezekana kuna fursa nyingi za kibiashara katika nchi zetu za SADC ambazo tukizitumia vizuri Zanzibar itapiga hatua kubwa za kimaendeleo kwa muda mfupi” Alieleza Mhe. Hemed

Akizungumizia juu ya Lugha ya Kiswahili Makamu wa Pili wa Rais alizitaka Taasisi zinazoshughulikia maendeleo ya lugha ya Kiswahili nchini kuanzisha mijadala na makongamano itakayoeleza jinsi ya kutumia fursa ya lugha hiyo , katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ajili ya kuwapatia wake fursa za ajira.

Alisema kwamba umefika wakati kuchangamkia fursa itokanayo na lugha ya Kiswahili akitolea mfano kwa baadhi ya nchi jirani kwa asilimia kubwa uchumi wao unachangiwa na kuuza Kiswahili nje ya nchi, Hivyo alisema ni vyema Kiswahili kiwe ni rasilimali inayochangia ukuaji wa uchumi wa Zanzibar kwa kuwanufaisha watu wake.

Pmoja na mambo mengine Mhe. Makamu wa Pili alitumia fursa hiyo kulikumbusha Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) kuzingatia maoni yaliotolewa kwenye ufungaji wa Kongamano la Kiswahili la mwaka jana lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul wakili ambapo serikali ilitoa maelekezo kwa baraza hilo kukistawisha Kiswahili na kukikuza nje ya nchi kwa faida ya wazanzibar na Watanzania kwa ujumla.

Aidha, aliwaomba washiriki wa kongamano hilo pamoja na wadau mbali mbali kutumia fursa ya mijadala inayoandaliwa kuishauri Serikali kuhusu njia bora zitakazotumika katika kuhakikisha vijana ambao ni wataalamu wa lugha hii waweze kuuzika katika soko la Jumuiya hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, aliendelea kuwanahisi washiriki wa kongamano hilo, kwa kupendekeza njia muwafaka zitakazotumika katika kutatua changamoto zinazoikabili Jumuiya hiyo sambamba na kueleza mafanikio yake ili wananchi waweze kuifahamu vyema Jumuiya pamoja na faida zake zinazoweza kupatikana.

Akimalizia houtuba yake Mhe. Hemed aliushukiru Uongozi wa SADC kwa kuonesha kuijali Zanzibar kwa kuona ipo haja kuandaa kongamano hilo la kitaaluma linawakutanisha wataalamu na wasomi wa Zanzibar ili kutoa maoni yao jambo ambalo limeonesha uzalendo na kukuwa kwa Demokrasia kwa Viongozi wa Jumuiya hiyo.

Nae, mwakilishi kutoka wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ambae pia ni Mkurugenzi wa Mambo ya nje Ofisi ya Zanzibar Masoud Balozi alikopongeza chuo cha Taifa SUZA kwa maandalizi mazuri ya kongamano hilo jambo ambalo litafanya Zanzibar kutambua fursa zinazopatina ndani ya Jumuiya ya SADC.

Alisema maadhimisho ya kutimia miaka 40 ya kuanzishwa SADC yanaadhimishwa kupitia nchi zote wanachama ambayo yanalenga kuenzi jitihada na mchango mkubwa uliotolewa na viongozi wan chi wanachama wa Jumuiya ya kusini mwa Afrika.

Alieleza kuwa, Tangu kuasisiwa kwa Jumuiya ya SADC ambapo Mwalimu Julius Nyerere alikuwa Mwenyekiti wa mwanzo Tanzania imetoa mchango mkubwa katika kupatikana kwa ukombozi wa nchi nyingi za Afrika.

Kwa Upande wake Makamu Mkuu wa chuo cha Taifa cha Zanzibar Dk. Zakia Abubakar alishukuru wizra ya mambo ya nje kwa kukichagua chuo cha Taifa Zanzibar kuwa mwenyeji wa kuandaa kongamano hilo.

Dk. Zakia alisema kufanyika kwa kongamano hilo katika chuo hicho kimetoa fursa ya kukitangaza zaidi chuo pamoja na kutoa fursa za kitaaluma kutoka SADC na kuahidi kuwa chuo cha SUZA kitakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu yoyote yanayotolewa na serikali kwa lengo la kuleta maendeleo ya nchi.

“Chuo kina wataalamu kupitia fani mbali mbali ambazo zitaweza kusaidia kukuza maendeleo ya Jumuiya hiyo” Alisema Dk. Zakia

Ujumbe wa Mwaka huu unasema Miaka 40 ya Jumuiya na Maendeleo ya Kiuchumi ya Mataifa ya Kusini na Mashariki wa Bara la Afrika {Sadc} ni kuimarisha Amani, Usalama na kuhamasisha Maendeleo na Ustahamilivu kati ya Changamoto inayoikabili Dunia.

Read 33 times Last modified on Saturday, 29 May 2021 14:05
Rate this item
(0 votes)

Toa Maoni yako hapa

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.

Mawasiliano

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.

Mtaa wa Vuga

S.L.P 239

Simu: +255 242231126

Nukushi (Fax): +255 242233788