Print this page
ACHENI KUWASUMBUA WAWEKEZAJI MHE. HEMED
20 Jul 2021

ACHENI KUWASUMBUA WAWEKEZAJI MHE. HEMED

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewagiza watendaji wa taasisi za serikali kuacha mara moja tabia ya kuwazungusha wawekezaji walioonesha njia ya kuwekeza Zanzibar ili kutoa fursa kwa nchi kupiga hatua za kimaendeleo.

Mhe. Hemedi ametoa onyo hilo wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo linalojengwa kiwanda cha kutengeneza  maji kinachojengwa katika eneo la Chamanangwe wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema jambo la kuwazungusha wawekezaji walioonesha nia ya kuwekeza katika ardhi ya Zanzibar halikubaliki, na serikali inayongozwa na Dk. Hussein Mwinyi haitolifumbia macho kwani kufanya hivyo kunalenga kurejesha nyuma azma ya serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Mhe. Hemed amefafanua kwamba endapo serikali itagundua  kuna taasisi inazorotesha kasi ya maendeleo ya serikali ya awamu ya nane, basi hatua za haraka za kuwaondosha wasimamizi wa taasisi hizo zitachukuliwa.

Akizungumzia faida zinazopatikana katika uwekezaji Makamu wa Pili wa Rais amesema kupitia uwekezaji serikali unapata uwezo wa kutatua changamoto mbali mbali ikiwemo masuala ya huduma za jamii.

Nae, Muwekezaji anaejenga kiwanda hicho cha maji cha AMOS INDUSTRY LIMITED Bw. Husamudin Ali Mussa ameipongeza serikali ya mapinduzi Zanzibar kwa jitihada zake kwa kuwapa kipaumbele wawekezaji kuwekeza jambo ambalo linatia moyo na wawekezaji wengi wameanza kujitokeza.

Bw. Husamudin amemueleza Makamu wa Pili wa Rais ujenzi wa kiwanda hicho unaondelea sasa unatarajiwa kukamilika  ndani ya kipindi cha miezi mitatu,huku wakiwa tayari wameshaagiza vifaa kwa ajili ya kufanya kazi katika kiwanda hicho.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa  Mamlaka ya kukuza  uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Sharif Ali Sharif amemueleza Makamu wa Pili wa Rais kukamilika kwa kiwanda hicho kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa utekelezaji wa Ilani ya chama cha mapinduzi kwa kufikia lengo la kutoa ajira laki Tatu kwa vijana wa Zanzibar.

Bw. Sharif amemuomba Makamu wa Pili wa Rais kupitia serikali kuangalia namna bora ya kulinda soko la ndani kwa wawekezaji walioamua kuwekeza Zanzibar kwani kwa muda mrefu sasa kumekuwa na changamoto ya ushindani wa soko kwa waingizaji wa bidhaa kutoka nje ya Nchi.

Last modified on Thursday, 05 August 2021 16:56