SMZ KUPOKEA MSAADA WA CHANJO  YA COVID-19
22 Jul 2021

SMZ KUPOKEA MSAADA WA CHANJO YA COVID-19

Jumla ya chanjo laki moja (100,000) zinatarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya Jamhuri ya watu wa China.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameleza hayo Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar wakati akipokea Stakabadhi ya msaada huo wa chanjo kutoka kwa Balozi Mdogo wa China anaefanyia kazi zake Zanzibar Bwana Zhang Zhisheng.

Mhe. Hemed amesema chanjo hizo aina ya SINOVAC zinategemewa kuwasili Zanzibar ndani ya muda baada ya kupokea Stakabadhi na mara baada ya kuwasili Zanzibar zinatakibidhiwa kwa Wizara ya Afya ikiwa ndio wizara yenye dhamana na musuala ya Afya.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itapokea chanjo hizo ikiwa ni katika juhudi za kujikinga na Maradhi ya Covid 19 kwa lengo la kuwakinga wananchi wake kutokana na virusi vinavyosababisha maradhi hayo.

Akizungumzia Ubora wa chanjo hiyo Makamu wa Pili wa Rais amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Chanjo hizo zipo salama kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani kuruhusu kutumika.

Katika hatua nyengine Mhe. Hemed ameendelea kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kuendelea kuunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika Sekta ya Afya akitolea mfano misaada mbali mbali inayotolewa na Nchi hiyo katika Hospitali na Mnazi Mmoja na ya Hospital ya Abdallah Mzee kwa Upande wa Pemba.

Amesema mashirikiano hayo yanaonesha ukaribu na udugu kati ya nchi hizo mbili yaliyoasisiwa kwa muda mrefu sasa ambapo hadi sasa China na Zanzibar zinashirikiana kupitia sekta tofauti.

Nae Balozi Mdogo wa China Bwana Zhang Zhisheng amesema China imejipanga kutoa chanjo ili kusaidia kinga dhidi ya covid 19 na alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa chanjo hizo ni salama kutokana na kupatikana kwa ruhusa ya kimatumizi kutoka  Shirika la Afya Duniani (WHO).

Aidha, Bwana Zhang Zhisheng amlimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Nchi ya China itaendeleza mashirikiano yaliyopo baina yao ili kuisaidia  Zanzibar kukuza uchumi wake ambapo serikali ya Jamuhuri ya watu wa China imejipanga kuisaidia Zanzibar katika kuwekeza kwenye Sekta ya Viwanda jambo ambalo litasadia kuinua uchumi wa zanzibar na watu wake.

Last modified on Monday, 09 August 2021 12:03

Mawasiliano

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.

Mtaa wa Vuga

S.L.P 239

Simu: +255 242231126

Nukushi (Fax): +255 242233788