Super User

Super User

Jumla ya chanjo laki moja (100,000) zinatarajiwa kukabidhiwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwa ni msaada kutoka Serikali ya Jamhuri ya watu wa China.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameleza hayo Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar wakati akipokea Stakabadhi ya msaada huo wa chanjo kutoka kwa Balozi Mdogo wa China anaefanyia kazi zake Zanzibar Bwana Zhang Zhisheng.

Mhe. Hemed amesema chanjo hizo aina ya SINOVAC zinategemewa kuwasili Zanzibar ndani ya muda baada ya kupokea Stakabadhi na mara baada ya kuwasili Zanzibar zinatakibidhiwa kwa Wizara ya Afya ikiwa ndio wizara yenye dhamana na musuala ya Afya.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itapokea chanjo hizo ikiwa ni katika juhudi za kujikinga na Maradhi ya Covid 19 kwa lengo la kuwakinga wananchi wake kutokana na virusi vinavyosababisha maradhi hayo.

Akizungumzia Ubora wa chanjo hiyo Makamu wa Pili wa Rais amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa Chanjo hizo zipo salama kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani kuruhusu kutumika.

Katika hatua nyengine Mhe. Hemed ameendelea kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kuendelea kuunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika Sekta ya Afya akitolea mfano misaada mbali mbali inayotolewa na Nchi hiyo katika Hospitali na Mnazi Mmoja na ya Hospital ya Abdallah Mzee kwa Upande wa Pemba.

Amesema mashirikiano hayo yanaonesha ukaribu na udugu kati ya nchi hizo mbili yaliyoasisiwa kwa muda mrefu sasa ambapo hadi sasa China na Zanzibar zinashirikiana kupitia sekta tofauti.

Nae Balozi Mdogo wa China Bwana Zhang Zhisheng amesema China imejipanga kutoa chanjo ili kusaidia kinga dhidi ya covid 19 na alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa chanjo hizo ni salama kutokana na kupatikana kwa ruhusa ya kimatumizi kutoka  Shirika la Afya Duniani (WHO).

Aidha, Bwana Zhang Zhisheng amlimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Nchi ya China itaendeleza mashirikiano yaliyopo baina yao ili kuisaidia  Zanzibar kukuza uchumi wake ambapo serikali ya Jamuhuri ya watu wa China imejipanga kuisaidia Zanzibar katika kuwekeza kwenye Sekta ya Viwanda jambo ambalo litasadia kuinua uchumi wa zanzibar na watu wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza tume ya taifa ya uchaguzi zanzibar (ZEC) kwa kazi nzuri waliofanya ya kukamilisha vyema zoezi la uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka jana.

 

Mhe. Hemed ameleza hayo wakati akipokea ripoti ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2020 iliowasilishwa na Mwenyekiti wa tume hiyo akiambatana na wajumbe waliofika Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.

 

Amesema Tume ya taifa ya uchaguzi Zanzibar imefanya kazi zake kwa uweledi na umahiri kutokana na kuzingatia sheria zinavyowaelekeza jambo ambalo limesaidia wananchi kujenga Imani dhidi ya watendaji wa tume hiyo.

 

Aliwahakikishia kwamba yeye akiwa mtendaji mkuu wa shughuli za serikali ataendelea kutoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika katika kufanikisha kazi za tume kutokana na Imani kubwa alionayo kwa viongozi wa tume.

 

Ameleza licha ya changamoto zilizosababishwa na baadhi ya wanasiasa kutaka kuvuruga zoezi hilo lakini ubobezi na ufanisi wa watendani wa tume wakiongozwa na Makamishna, wameweza kuzikabili pamoja na kuzitatua changamoto hizo jambo ambalo limeonesha utayari na uweledi waliokuwanao watendaji wake.

 

Akiwasilisha ripoti hiyo Mwenyekti wa Tume ya taifa ya Uchaguz Zanzibar (ZEC) Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Tume imeamua kukabidhi ripoti kwake kwa kutambua kuwa Makamu wa Pili wa Rais ndio kiongozi mkuu wa shughuli za Serikali lakini kimuundo tume ya uchaguzi  Zanzibar ipo chini ya Ofisi ya Makamu  wa Pili wa Rais.

 

Mwenyekiti huyo wa Tume ya uchaguzi amemueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa tume inatoa shukrani zake za dhati kwa serikali kwa ushirikiano wake katika kuiwezesha tume hiyo kufanikisha kazi zake.

 

Ripoti hiyo iliowasilishwa kwa Makamu wa Pili wa Rais imeelezea kwa kina hali ya Uchaguzi ilivyo kabla, wakat na baada ya uchaguzi, ikihusisha mafaniko na baadhi ya changamoto zilizoikumba tume hiyo

Kuwepo kwa ubunifu wa mambo mbali mbali yenye maslahi na Zanzibar ni jambo jema linalokuza uzalendo kwa wananchi wake pamoja na kutanua wigo kimataifa katika kuitangaza Nchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, ametoa kauli hiyo alipokutana  na kamati ya Zanzibar International Marathon walipofika Ofisini kwake Vuga kwa lengo la kumkabidhi vifaa vya ushiriki katika wa mashindano hayo.

Makamu wa Pili wa Rais amesema mashindano hayo kuitangaza Zanzibar kiutalii ambapo wageni watakaoshiriki katika mashindano hayo  wataweza kujifunza mambo mengi kutokana na upekee wa utamaduni wa kizanzibar.

Aidha, Amepongeza Bw. Salim Kike mtangazaji wa Shika la BBC Uwengereza kwa jitihada zake akiwa kama balozi kwa kuitanga vyema Zanzibar na Tanzania kwa ujula katika anga za kimataifa.

Nae Mwenyekiti wa kamati hiyo Ndugu Hassan Suleiman Zanga amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa juhudi zake alizozifanya hasa katika kuwahamasisha viongozi mbali mbali sambamba na  wito wake alioutoa kwa taasisi mbali mbali nchini kuweza kuunga mkono jambo hilo, ambapo mashirika na tasisi tofauti yamejitokeza kuunga mkono.

Mbio hizo za Zanzibar International Marathonzinatarajiwa kufanyika  july 18 2021, ambapo hadi sasa jumla ya watu 12,000 wamekwisha kujisajili. 

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amepokea zawadi za washindi wa mashindano ya yamle yamle cup zilizotolewa na Bwana Mohamed Raza Mwenyekiti wa Kampuni ya ZAT.

Mhe. Hemed ameitaka wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kujitathmini kupitia mashindano hayo ili kurejesha hadhi ya soko visiwani Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk.Hussen Ali Mwinyi inathamini mchango unaotolewa na Viongozi wa Dini  hali inayopelekea kudumisha Amani na Utulivu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla ameeleza hayo katika mkutano uliojadili nafasi ya  Viongozi wa Dini  katika kudumisha Amani na utulivu ulifanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakili Kikwajuni Jijini Zanzibar

Ameeleza kuwa,uwepo wa Amani na utulivu unaochangiwa na Viongozi wa Dini umesaidia kuwavutia Wawekezaje tofauti jambo ambalo limepelekea kwa kupatikana kwa nafasi nyingi za ajira kwa jamii na kufanikisha kufikiwa kwa lengo la Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025.

Alifafanua kwamba,Viongozi wa Dini wamekuwa na moyo wa kijitolea katika kuhakikisha Amani ya Nchi inakuwepo muda wote kutokana na kazi nzuri walioifanya ya kuhakikisha Amani kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi Mhe. Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi ameeleza kuwa taifa limejaaliwa Rehma na Baraka kutoka kwa Allah (S.W.) Kwa kuwa na Amani Jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa Waumini na Wananchi kutekeleza ibada.

Akitoa salamu za Shirika la Umoja wa Mataifa  linaloshughulikia watoto duniani (UNICEF)  Naibu Muwakilishi wa UNICEF anaeshuhulikia Operesheni  Bw. Lawrence Oundo ameipongeza Serikeli ya Mapinduzi ya Zanzibar  kupitia Afisi ya Mufti kwa hatua wanazoendelea kuchukua katika kuwapatia watu  taaluma juu ya masuala mbalimbali ikiwemo elimu ya kujikinga na kipindupindu, COVID-19 pamoja na Kupiga vita vitendo vya udhalilishaji.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wananchi kutoa ushirikiano katika kupiga vita dhidi ya uwingizaji, usambazaji na utumiaji madawa ya kulevya Nchini.

Mhe. Hemed ametoa wito wakati akitoa salamu zake kwa waumini wa Masjid Nouri Kombeni Mkoa wa Mjini Magharibi mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema umefika wakati Wananchi wa Zanzibar kuungana pamoja katika kupiga vita Madawa ya kulevya ili kuiokoa jamii na athari zitokanazo na madawa ya kulevya.

Akigusia suala la Sheria juu ya madawa ya kulevya Makamu wa Pili wa Rais  alisema Serikali haitasita kuifanyia marekebisho Sheria hiyo kama ilivyochukua hatua katika Sheria nyengine kwa lengo la kuwabana wahalifu wa vitendo hivyo.

Akizungumzia juu ya maradhi ya Covid 19 aliitaka jamii kuendelea kuchukua tahadhari juu ya wimbi la tatu linalotarajiwa kuikumba dunia  kwa kutumia njia ya kunawa mikono kwa kutumia maji tiririka, kuepuka mikusanyiko pamoja kuvaa barakoa.

Mapema Khatibu wa Msikiti huo Sheikh Abdallah Juma Mussa aliwataka Waumini wa dini ya Kiislamu kuijenga jamii katika maadili mazuri  ili kupunguza vitendo viovu ikiwemo matumizi ya dawa za kuelvya.

Wananchi wametakiwa kujisajili katika ushiriki wa Mashindano ya mbio za Zanzibar International Marathon zinazotarajiwa kufanyika julai 18 mwaka huu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito huo alipokutana na kufanya mazungumzo na kamati ya maandalizi ya mashindano hayo walipofika Ofisini kwake Vuga Jijni Zanzibar.

Amesema kwa kuwa mashindano hayo yamepata Baraka za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la  Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi itatoa taswira njema endapo watu wengi watajitokeza kushiriki ikiwemo wenyeji na wageni kutoka mataifa mengine.

Akigusia suala la udhamini wa mashindano hayo Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali itazungumza na Makampuni mbali mbali pamoja na mashirika yaliyopo Zanzibar ili kushiriki kikamilifu.

Nae Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale ambae pia ni Kaimu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Leila Muhamed Mussa amesema kuwepo kwa mashindano hayo ya Marathon kutasaidia kuunga mkono azma ya Rais Dk. Mwinyi ya kukuza Uchumi wa Zanzibar hasa kupitia Uchumi wa Buluu ambapo Sekta ya Utalii ni moja kati ya maeneo ya uchumi huo.

Nao Viongozi wa Kamati hiyo wakiongozwa na Hassan Suleiman Zanga wamemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa lengo la Marathon hiyo kufanyika Zanzibar ni kuhamasisha utalii hasa katika kipindi hichi cha mripuko wa maradhi ya covid 19 ambapo inaonekana sekta hiyo kusuasua katika mataifa mbali mbali.

Makamu wa wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali itaendelea kuwahudumua majeruhi waliopata ajali Mkoani Shinyanga ilitokea tarehe 02, Juni mwaka huu.

Mhe. Hemed alieleza hayo leo alipofika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salam kuwajulia hali majeruhi hao pamoja na kuwafariji.

Alisema Serikali zote mbili zitaendelea kushirikiana kwa karibu katika kuhakikisha afya za majeruhi hao ambao ni Watumishi wa Serikali ya Mapinduzi  ya Zanzibar waliokuwa ni Wanafunzi  wa Kada ya Afya katika Chuo cha BUGEMA UNIVERSITY  nchini Uganda.

Makamu wa Pili wa Rais aliwataka madaktari hospitalini hapo kuendelea kuwapatia huduma bora majeruhi hao na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Mratibu wake anaesimamia shughuli za Serilikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili Wa Raisi Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi aliopo Dar es salam ataendelea kutoa ushirikiano unaohitajika.

Aidha, amewaagiza madktari wanaowasimia majeruhi kutofanya haraka ya kuwatoa wagongwa mpaka pale watakapojiridhisha kuwa afya zao zimeimarika na Serikali itaendelea  kugharamia matibabu yao.

“Kamwe  isitokee sababu yoyote ile itakayopelekea wagonjwa wetu hawa kukosa huduma” Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar imefarajika na jitihada zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Madaktari katika kuhakikisha Afya za wagongwa zinaimarika siku hadi siku.

Nae Daktari  Bingwa wa masuala ya Mifupa katika hospitali ya Taifa Muhimbili  Dk. Victoria Munthali  alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais kuwa  uongozi wa Hospitali kwa kushirikana na madaktari watendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa mpaka pale afya zao zitakapotengemaa sawa sawa.

Kwa  upande wao majeruhi wanaopata matibabu katika hospitali ya Taifa Muhimbili walimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa  wanamshukuru sana  Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi pamoja na wasaidizi wake kwa ushirikiano waliowapatia tangu kutokea kwa ajali hadi sasa.

Walisema wanaridhika na huduma wanazopatiwa kutoka kwa madaktari pamoja na Wauguzi  na kueleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni kupata maamuzi lakini Afya zao zinaendelea kuimarika vizuri.

Makamu wa Pili wa Rais amefika Hospitalini hapo akitokea Mkoani Dodoma  kushiriki kikao cha Kamati Kuu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Sera, Uratibu na  Baraza la Wawakilishi Dkt  Khalid  Salum Mohammed, amewataka Wawakilishi na Madiwani kuwa makini na matumizi ya  fedha za mfuko wa jimbo kuzitumia kama zilivyokusudiwa.

Ameyasema hayo wakati akifungua Kikao cha kupokea na kukusanya maoni juu ya  Sheria namba 4 ya mwaka 2012 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 ya mfuko wa maendeleo  ya jimbo kilichofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa  Abdulwakil Kikwajuni.

 Amesema kuwa  katika uibuaji wa Miradi ya Maendeleo ya  jimbo   kwa kutumia fedha hizo  ni vyema Waheshimiwa Wawakilishi wakawaachia Wananchi wenyewe  kuchagua miradi wanayo itaka  ambayo itawasaidi kukuza maendeleo katika maeneo yao.

Akimkaribisha mgeni Rasmi  katika kikao hicho Mkurugezi wa  Uratibu na shughuli za Serikali  Nd   Khalid Bakar Amran  amewataka Wawakilishi pamoja na Madiwani  ambao ni wadau wakubwa wa sheria  hiyo kutoa maoni yao yatakayo weza kuondosha changamoto zilizomo  ndani ya    sheria hiyo.

Nao, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakitoa Maoni yao katika kikao hicho   wamependekeza kuwa   ni vyema kuweza kuwapunguzia kazi  Wakurugenzi  na kuwataka  wabaki na  kazi  ya kushughulika na majukumu ya halmashauri    na kupendekeza   Wananchi  kuchagua    Diwani miongoni mwao kuwa msimamizi  wamiradi hiyo.

“Ni vyema  Serikali ikaangalia  kumpunguzia kazi mkurugenzi wa halmashauri  kwa kuenelea kufanya kazi nyengine  nakuangalia uwezekanano wakmchagua Diwani yoyote ambaye atapendekezwa na Kamati  kuweza kusimamia  miradi hiyo alisema Mwakilshi wa Jimbo  la Mkwajuni’ Sulubu Kidombo Amour.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Baraza la Biashara la  Afrika Mashariki na Jumuiya ya wafanyabiashara Zanzibar katika kuwaunganisha wafanyabiashara wake.

Rais Dk. Mwinyi ameleza hayo katika hotuba iliosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika kikao cha kujadili uimarishaji wa Biashara ndani ya Afrika Mashariki kikao ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Hotel ya Verde iliopo Mtoni.

Kupitia Mkutano huo Makamu wa Pili wa Rais amemueleza Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Dk. Peter Mutuku Mathuki kwamba wafanyabiashara wa Zanzibar ni waamifu wana uwezo mzuri kutokana na Zanzibar kuwa kitovu cha Biashara Afrika Mashariki kwa Karne nyingi sasa.

Amefafanua kuwa, wazanzibar wanajulikana kwa umahiri na ustadi wao katika sekta ya biashara na ujasiri wa kutanua biashara zao katika Pembe tofauti za dunia hivyo, ujio wa kiongozi huyo kutafungua milango Zaidi ya kuwaingiza wafanyabiashara wa Zanzibar katika nchi sita wanachama wa Jumuiya.

Akizungumzia suala la uwekezaji Mhe. Hemed aliwaeleza wafanyabiasha hao kwamba kwa sasa Zanzibar inadhamiria kuinua uchumi wake kupitia uchumi mpya unaofahamika kama Uchumi wa Buluu(Blue Economy) unaojumuisha Uvuvi wa bahari Kuu, Miundombinu ya Bandari na usafiri, mafuta na gesi, utalii na maeneo mengine.

Nae, Waziri wa Biashara na maenedeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban amewahakikishia wafanyabiashara wa Afrika Mashariki kuwa serikali kupitia wizara anayoisimamia itahakikisha nembo ya ZBS inatambulika ndani Jumuiya hiyo kwa lengo la kuwaondoshea wafanyabiashara wake vikwazo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dk.Peter Mathuki alisema ziara yake nchini Tanzania imeza matunda kwa kuonana na kubadilishana mawazo na Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. Samia Suhuhu Hassan ambapo Katibu Mkuu huyo alisisitiza lugha ya Kiswahili kupewa kipaumbele kutumika kwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar  Ali Suleman Amour amesema sekta binafsi inahitaji kuinuliwa ili kutoa manufaa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na fikra nzuri walizonazo wafanyabiashara ikiwemo masuala ya uajasiriamali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka wafanyabiashara wa soko la Kibandamaiti kuimarisha umoja na ushirikiano katika utendaji wa kazi ili kutengeneza mazingira mazuri katika biashara zao.

Mhe. Hemed alieleza hayo wakati alipofanya ziara katika soko la kibanda maiti kwa lengo la kuskiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara pamoja na kujionea hali halisi ya mwenendo wa biashara ndani ya soko hilo.

Akiyatembelea mabanda hayo waliopewa wafanyabiashara Makamu wa Pili wa Rais alionesha kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya watu waliopewa nafasi kwa ajili ya kuendesha biashara kuyatelekeza mane ohayo halio inayopelekea usumbufu kwa watu wengi.

Page 1 of 4

Mawasiliano

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.

Mtaa wa Vuga

S.L.P 239

Simu: +255 242231126

Nukushi (Fax): +255 242233788