KAMISHENI YA KUKABILIANA NA MAAFA ZANZIBAR:

Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar imeanzisha kwa Sheria ya Kukabiliana na Maafa Namb. 1 ya mwaka 2015 na inaongozwa na Mwenyekiti ambae ni Makamu wa Pili wa Rais ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais anakuwa Makamu Mwenyekiti. Wajumbe wa Kamisheni ni Mawaziri wote wa SMZ, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na Wakuu wa Mikoa. Katibu Mkuu wa Wizara inayosimamia maafa anakuwa ndie Katibu wa Kamisheni. Majukumu mahasusi ya Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa ni pamoja na:-

 • Kuhakikisha uwajibikaji wa taasisi muhimu katika utekelezaji wa Sheria ya Kukabiliana na Maafa Nam. 1 ya mwaka 2015;
 • Kuanzisha sera za kukabiliana na maafa, kanuni, mipango, mikakati na miongozo ili iweze kukabiliana na maafa kwa wakati na ufanisi;
 • Kuwezesha upatikanaji wa fedha na rasilimali nyengine wakati wa dharura na/au maafa;
 • Kusimamia utekelezaji wa mipango ya kukabiliana na maafa wakati wa maafa au dharura na kutoa amri au maelekezo yanayofaa kwa utekelezaji wa mpango huo;
 • Kuratibu huduma za utoaji wa misaada ya kibinadamu pamoja na hatua za kujiandaa katika kukabiliana na maafa;
 • Kuwa na jukumu la kusimamia na kuratibu kazi za kukabiliana na maafa nchini;
 • Kupendekeza utaratibu wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukabiliana na maafa;
 • Kuimarisha uwezo wa Serikali katika kusimamia hali za dharura na/au maafa;
 • Kuangalia uwezekano wa upatikanaji wa rasilimali ndani na nje ya Zanzibar ili kukabiliana na maafa kwa ufanisi;
 • Kuhakikisha utekelezaji wa sera za Serikali, sheria, mipango na kazi za kukabiliana na maafa zinaendana na makubaliano pamoja na mikataba ya Kikanda na Kimataifa;
 • Kuhakikisha kuwa taasisi za Serikali, Wilaya na Shehia zinakuwa na uwezo wa kukabiliana na maafa kupitia utoaji wa mafunzo na vifaa; na
 • Kufanya kazi yoyote ambayo Kamisheni itaona inafaa katika kutekeleza shughuli za kukabiliana na maafa.

Katika kutekeleza majukumu ya kila siku ya Kamisheni, imeanzisha Sekreterieti ya Kamisheni inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji. Sekreterieti ya Kamisheni ina Idara tatu (3) zinazotekeleza majukumu ya msingi na Idara mbili (2) ambazo zinazotekeleza majukumu yasiyo ya msingi ambazo ni Idara ya Elimu na Tafiti, Idara ya Mawasiliano na Tahadhari za Mapema, Idara ya Operesheni na Huduma za Kibinaadamu, Idara ya Mipango, Utawala na Rasilimali Watu na Ofisi ya Uratibu wa Maafa Pemba. Aidha, Kamisheni ina vitengo vikuu sita (6) ambavyo vinasimamiwa moja kwa moja na Mkurugenzi Mtendaji. Vitengo hivyo ni Kitengo cha Sheria, Kitengo cha Uhusiano, Kitengo cha Ukaguzi wa ndani, Kitengo cha Uhasibu, Kitengo cha Ununuzi na Ugavi na Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano.

Vilevile, katika muundo wa Kamisheni pia kuna Kamati za Kitaalamu ya Kitaifa, Wilaya na Shehia za Kukabiliana na Maafa.

Mawasiliano

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.

Mtaa wa Vuga

S.L.P 239

Simu: +255 242231126

Nukushi (Fax): +255 242233788