TUME YA UCHAGUZI YA ZANZIBAR:

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar inafanya kazi zake kwa mujibu wa Sheria ya Afisi ya Tume ya Uchaguzi Nam. 1 ya mwaka 2017 ina jukumu la kusimamia shughuli zote za uchaguzi nchini. Majukumu mahasusi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni pamoja na:-

  • Usimamizi wa jumla wa mienendo mizima ya Uchaguzi wa Rais, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Viongozi wa Serikali za Mitaa;
  • Kukuza na kuratibu elimu ya wapiga kura;
  • Kufanya mapitio ya idadi, majina na mipaka ya majimbo ya uchaguzi ya Zanzibar;
  • Kuandikisha wapiga kura na kuendeleza wa Daftari la kudumu la Wapiga Kura; na
  • Kuendesha na Kusimamia Kura ya Maoni.

Muundo wa Tume ya Uchaguzi unatokana na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 kifungu cha 119(1) ambao ni kama ifuatavyo:

  1. Mwenyeketi, anayeteuliwa na Rais ambaye ni mtu mwenye sifa za kuwa Jaji katika Mahkama Kuu au Mahkama ya Rufaa katika nchi za Jumuiya za Madola au mtu anaye heshimika katika jamii;
  2. Wajumbe wawili wanaotokana na mapendekezo ya kiongozi wa upinzani katika Baraza la Wawakilishi na kama hayupo, kwa mashauriano na vyama vya siasa;
  3. Wajumbe wawili wanatokana na kiongozi wa shughuli za Serikali kwenye Baraza la Wawakilishi;
  4. Mjumbe mmoja kutoka miongoni mwa majaji wa Mahkama Kuu, na
  5. Mjumbe mmoja anayeteuliwa na Rais kama atavyoona inafaa.

Vilevile, katika utekelezaji wa majukumu yake Tume imeundwa na divisheni saba ambazo wakuu wa divisheni hizo ndio wanaounda sekreterieti ya Tume na wanakuwa ni washauri wakuu wa Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye ni Katibu wa Tume pia Mkurugenzi huyo ndiye mkuu wa Sekretarieti ya Tume. Divisheni hizo ni Afisi ndogo Pemba, Divisheni ya Utawala, Divisheni ya Uchaguzi, Divisheni ya Sheria, Divisheni ya Elimu ya Wapiga Kura, Divisheni ya Teknolojia ya Habari na Divisheni ya Fedha na Ukaguzi. Aidha, pamoja na divisheni hizo, Ofisi pia ina vitengo viwili (2) ambavyo ni Kitengo cha Ununuzi na Ugavi na Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani.

Mawasiliano

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.

Mtaa wa Vuga

S.L.P 239

Simu: +255 242231126

Nukushi (Fax): +255 242233788