TUME YA KITAIFA YA KURATIBU NA UDHIBITI WA DAWA ZA KULEVYA:

Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar, imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria namba 9 ya 2009, Sheria za Zanzibar (The Prevention of Illicit Drugs and Trafficking Act, 2009). Kwa mujibu wa kifungu cha 4 (1) cha Sheria hiyo kinataja majukumu ya Tume kuwa ni Kuiainisha, Kuifafanua, Kuitangaza na Kuiratibu Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Matumizi na Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya.

Aidha, kifungu cha 7 (1) cha Sheria hiyo kinataja kazi za Tume kama zifuatazo:

 • Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Udhibiti wa Dawa za Kulevya;
 • Kusimamia utekelezaji wa mikataba na itifaki za Kimataifa katika udhibiti wa dawa za kulevya;
 • Kupitia sheria na kanuni za udhibiti wa dawa za kulevya na kupendekeza marekebisho ili ziendane na wakati;
 • Kuimarisha na kuendeleza jitihada za kuzuia matumizi ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa hizo;
 • Kuanzisha mfumo wa ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya;
 • Kuendeleza mipango ya tiba na urekebishaji wa tabia za waathirika wa dawa za kulevya;
 • Kufanya tafiti kuhusu ukubwa wa tatizo la dawa za kulevya;
 • Kutoa mafunzo kwa watu wanaojihusisha na udhibiti wa matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya;
 • Kuimarisha na kuendeleza uhusiano wa Kimataifa katika udhibiti wa dawa za kulevya;
 • Kuratibu na kusaidia shughuli zinazofanywa na asasi zisizokuwa za kiserikali (NGOs) na vikundi mbali mbali vya kijamii vinavyoshiriki katika kupiga vita dawa za kulevya;
 • Kuandaa ripoti ya mwaka inayoelezea hali halisi ya tatizo la Dawa za Kulevya na kutoa mapendekezo yatakayoboresha vita dhidi ya Dawa za Kulevya;

Taasisi hii inaongozwa na Mwenyekiti ambae pia ni Makamo wa Pili wa Rais Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi. Wajumbe wa Tume wanatoka taasisi mbalimbali zinazohusika kwa namna moja ama nyengine na mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya au zinahusika na matibabu kwa watumiaji wa dawa hizo. Wajumbe hao ni kama wafuatao:

 1. Mwenyekiti – ambae anateuliwa na Mheshimiwa Rais
 2. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais. (Mjumbe) ambae pia ni Makamu Mwenyekiti.
 3. Waziri anaeshughulikia masuala ya Afya (Mjumbe)
 4. Waziri anaeshughulikia Vijana (Mjumbe)
 5. Waziri anaeshughulikia Elimu (Mjumbe)
 6. Waziri anaeshughulikia Bandari na Viwanja vya Ndege (Mjumbe)
 7. Waziri anaeshughulikia Utalii (Mjumbe)
 8. Waziri anaeshughulikia Tawala za Mikoa (Mjumbe)
 9. Waziri anaeshughulikia Sheria (Mjumbe)
 10. Mkurugenzi wa Mashtaka (Mjumbe)
 11. Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar (Mjumbe)
 12. Kamishna wa Polisi Zanzibar (Mjumbe)
 13. Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa Zanzibar (Mjumbe)
 14. Naibu Mkurugenzi wa Forodha Zanzibar (Mjumbe)
 15. Mkemia Mkuu wa Serikali (Mjumbe)

Na wajumbe wawili ambao watateuliwa na Waziri husika ambao kwa sasa ni:-

 1. Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Rushwa (Mjumbe)
 2. Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Mjumbe)
 3. Na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ambae anakua Katibu wa Tume.

Aidha, katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku, Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti Dawa za Kulevya inafanya kazi kupitia Sekretarieti ya Tume inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji ambae ndie Afisa Mtendaji Mkuu mwenye dhamana ya utendaji wa kazi hizo. Sekretarieti hiyo, inaundwa na Idara kuu tatu, ambazo ni Idara ya Kinga Tiba na Marekebisho ya Tabia, Idara ya Uchunguzi na Udhibiti, Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, na Ofisi Kuu Pemba.

Mawasiliano

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.

Mtaa wa Vuga

S.L.P 239

Simu: +255 242231126

Nukushi (Fax): +255 242233788